Advertisements

Friday, August 26, 2016

UPDATES: POLISI WAUA MAJAMBAZI ENEO LA VIKINDU LEO

MAJIBIZANO ya risasi baina ya polisi na majambazi yaliyodumu kwa takribani saa saba kuanzia saa 8:20 usiku wa kuamkia leo Mtaa wa Vikindu Mashariki, Mkuranga mkoani Pwani, yamesababisha vifo vya watu wawili, akiwemo askari Polisi na mtu mwingine anayedaiwa kuwa ni mtuhumiwa wa ujambazi.
Mbali ya milio ya risasi, mtaa huo pia ulitanda moshi kutokana na mabomu ya machozi yaliyopigwa mfululizo na kuibua taharuki kubwa kwa wakazi wake. Mmoja wa majirani katika nyumba iliyozingiwa waliyoishi watuhumiwa, Mjenge Faki alisema walishtuka usingizini na kuanza kusikia milipuko ya risasi na ghafla wakaanza kutokwa na machozi kufuatia hewa hiyo ya machozi kuanza kusambaa.
Katika majibizano hayo, askari aliyekuwa katika mapambano na mtuhumiwa, walikufa papo hapo. Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi, licha ya kuwepo eneo la tukio, hakuwa tayari kuzungumzia lolote, akisema mwenye jukumu la kuzungumzia tukio hilo ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.
Naye Kamanda Sirro akizungumzia hilo, alisema taarifa kamili za tukio hilo zitatolewa leo, kwani bado wanakusanya taarifa kuhusiana na tukio hilo. Lakini Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema katika mapambano hayo, Jeshi la Polisi limepoteza askari mmoja, lakini bado liko imara na litaendelea kuwasaka wahalifu popote watakapokuwepo.
“Askari wetu akiwa katika shughuli zake za kupambana na majambazi ameuawa hapa leo usiku, ni tukio baya katika wilaya yetu, katika mkoa wetu na ni tukio baya sana katika nchi yetu. Hawa ni wahalifu, lakini mbaya zaidi hata familia na watoto wao inaaminika wana mafunzo maalumu ya kulinda wazazi wao ambao ni wahalifu,” alisema Ndikilo.
Aliongeza kuwa, kama wahalifu hao walidhani kwa kuua askari watakuwa wametimiza malengo yao, basi wamechelewa kwani watawawinda popote pale watakapokwenda. Kwa mujibu wa Faki, milio ya risasi na mabomu ilisikika katika nyumba inayosadikiwa kumilikiwa na mkazi wa Temeke, aliyetajwa kuwa ni Salum Kingungo, majira ya saa 8:20 usiku.
“Tulianza kusikia kama watu wanakimbizana kutoka eneo la juu barabarani na kelele hizo zikaja kuishia ndani ya nyumba hii ambapo yalianza kusikika majibizano ya risasi baina ya watu walioko nje na mingine kutoka ndani, lakini hatukuweza kujua kinachoendelea kwani tulijawa na hofu kubwa ya kinachoendelea,” alisema Faki.
Alisema alishindwa kutoka nje na hata walipofanikiwa kubaini kuwa ni askari, hawakuruhusiwa kutoka nje hadi ilipotimu saa tano asubuhi. HabariLeo ilifika eneo la tukio na kushuhudia idadi kubwa ya polisi waliovalia sare wakiwa na silaha za aina mbalimbali huku wakiwa wametanda katika eneo hilo wakiongozwa na Kamanda Mushongi.
Katika majibizano hayo ya risasi na mabomu, nyumba inayodaiwa yalikuwa makazi ya watuhumiwa hao, iliharibiwa vibaya. Baada ya hali kutulia, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo akiwa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani, alipata fursa ya kuzungumza na wananchi.
Baada ya kutembelea nyumba hiyo na kujionea hali halisi ilivyokuwa, aliwataka wananchi wa Mkuranga na mkoa wa Pwani kwa ujumla kuwa watulivu kwani serikali imejipanga kupambana na watu wachache wasio waaminifu, ambao wamekuwa wakivuruga amani na utulivu.
Aliwataka wananchi wenye taarifa zozote za uhalifu kufika ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mkuranga au ofisini kwake huku akiahidi kutoa zawadi ya Sh 300,000 kwa mtu atakayewezesha kukamatwa kwa wahalifu. Pia aliwataka kuimarisha ulinzi, ikiwa pamoja na kujiwekea utaratibu wa kufahamu nyendo za majirani zao.
Taarifa za awali kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Vikindu Mashariki, Mohammed Maundu alisema watu saba kutoka katika familia hiyo wanashikiliwa na Polisi ambapo kati yao wanawake wawili, mwanamume mmoja na watoto ni wanne akiwemo mwenye umri wa miezi miwili.
Wananchi wa eneo hilo walisema tangu wakazi hao wahamie katika nyumba hiyo miaka mitatu iliyopita, hawajawahi kuwaona nje wanawake hao na hata wakionekana ni nadra sana na muda mwingi wamekuwa wakiwaona wanaume wawili na watoto hasa wa kiume mwenye umri wa miaka kati ya saba na 10, ambaye alikuwa haendi shule, lakini akiwa anatumwa dukani na kurudi ndani.
“Sisi hata siku moja hatujawahi kuwaona wamama wenzetu wa nyumba hii, lakini mara zote tukiona wanaume wawili mmoja mweupe na mwingine mweusi mfupi wakichota maji na kununua mahitaji tu lakini tulikuwa hatuwaelewi kutokana na mwonekano wao,” alisema mmoja wa majirani, Bahati Mawinga.
Baadhi ya watoto na akinamama waliokuwa eneo la tukio, walisema moshi wa kuwasha uliotokana na mabomu ya machozi ulisababisha watoto kulia usiku kucha na kutapika. Tukio la Vikindu limekuja siku nne baada ya askari Polisi wanne waliokuwa wanaingia kazini, kuuawa katika shambulio lililofanyika katika eneo la benki ya CRDB, Mbande, wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

No comments: