Advertisements

Monday, November 23, 2015

Magufuli alivyomsasambua Kikwete kweupe

Uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kueleza kwa kina namna safari holela za nje ya nchi zinavyoligharimu taifa mabilioni ya fedha, umeianika wazi Serikali iliyopita ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wachambuzi walisema kuwa ujasiri wa Rais Magufuli kueleza bila kificho jinsi safari za nje zinavyogharimu taifa kabla ya kutangaza msimamo mkali wa kuzidhibiti umedhihirisha pasi na shaka kuwa rais huyo mpya amedhamiria kubana matumizi holela ya fedha za serikali na badala yake kuzielekeza katika shughuli za maendeleo kwa nia ya kuboresha maisha ya Watanzania.

Hata hivyo, watu hao waliozungumza na Nipashe kwa sharti la kutotajwa majina walisema hatua hiyo ya Magufuli, imeibua jambo jingine, ambalo ni lile la kuanika udhaifu wa serikali iliyopita katika kusimamia eneo hilo.

Wakati akilihutubia Bunge la 11 Ijumaa iliyopita kisha kulizindua rasmi, Rais Magufuli aliwataka wabunge na Watanzania wote wamuunge mkono katika uamuzi wake wa kupiga marufuku safari holela za nje huku akisisitiza kuwa kwa kufanya hivyo, fedha nyingi zinazopotea zinaweza kutumiwa katika kuboresha huduma za jamii.

Akitaja kwa mifano jinsi safari hizo za vigogo nje ya nchi zinavyoligharimu taifa, Magufuli alisema katika mwaka wa fedha 2013/2014 na 2014/2015 peke yake, taifa lilitumia Sh. bilioni 356.324 kugharimia safari hizo; kiasi ambacho kwa maelezo yake, kingetosha kujenga barabara ya lami ya urefu wa kilomita 400 na pia kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya maji, elimu na afya.

Alisema mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo ulikuwa ni tiketi za ndege (Air ticket) Sh. bilioni 183.160, mafunzo nje ya nchi Sh. bilioni 68.612 na posho za kujikimu (Per Diem Foreign) Sh. bilioni 104.552.

Magufuli alizitaja wizara na taasisi za umma zilizoongoza kwa kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari za nje ya nchi kuwa ni Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, sasa safari hizo ni marufuku na pale inapolazimu, ni lazima kibali kitoke kwake au kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, na kwamba, kuanzia sasa watakaokuwa wakijumuishwa kwenye misafara ya lazima nje ya nchi ni watu muhimu tu wanaohitajika katika safari husika.

“Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya chini, kama afya, maji, elimu na umeme. Mfano, fedha hizi zingetosha kutengeneza kilomita 400 za barabara za lami. Tujiulize, zingeweza kutengeneza zahanati ngapi? nyumba za walimu ngapi? Madawati mangapi?” alihoji Rais Magufuli wakati akielezea suala hilo bungeni na kuongeza:

“Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mtuelewe na mtuunge mkono.”

ALIVYOISASAMBUA SERIKALI YA JK
Uchunguzi wa Nipashe uliohusisha rejea mbalimbali ikiwamo hotuba ya Rais Magufuli mwishoni mwa wiki umebaini kuwa misafara ya mara kwa mara ya viongozi mbalimbali kwenda nje ya nchi ilikuwa ikiligharimu taifa kwa kiasi kikubwa kwani ni kweli, kama alivyosema Rais Magufuli, fedha hizo zingefanya mambo mengi kwa manufaa ya nchi badala ya kunufaisha vigogo wachache.

Uchunguzi huo umebaini kuwa wakati fedha nyingi zikitumika kwa safari hizo, bado hali ni mbaya katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii; mambo ambayo Magufuli amesisitiza kuwa kamwe hatakubali kuyaruhusu katika serikali yake ya awamu ya tano.

“Ingawa Rais Magufuli hakuwa na lengo la kuanika udhaifu wa serikali iliyopita katika kusimamia matumizi ya fedha za umma, ukweli unabaki palepale kuwa Rais Magufuli ameianika sana serikali ya Kikwete,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe na kuongeza:

“Kwa mfano, Rais Magufuli hakuitaja Ikulu katika hotuba yake… lakini anapoitaja Mambo ya Nje kuwa ni miongoni mwa Wizara zilizokuwa vinara kwa safari za nje, ni wazi kwamba wanufaika wakuu ni pamoja na maafisa waliokuwa wakisafiri kila mara kupitia taasisi hiyo nyeti.

Huu ni ujasiri wa hali ya juu wa Magufuli na ambao unatoa matumaini ya kufanyika kazi makini ya kuboresha maisha ya Watanzania, siyo maneno matupu.”
Mchambuzi mwingine aliiambia Nipashe kuwa kwa mtazamo wake, ni kufuru kubwa kuona wakubwa wakipishana hewani kila uchao huku wananchi wakiteseka kwa kukosa baadhi ya huduma muhimu zinazopaswa kutolewa na serikali yao.
“Hata aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (Bernard Membe) analijua hilo.

Hali ilikuwa mbaya sana. Ni vizuri Magufuli amelivalia njuga jambo hili mapema kwani ni eneo mojawapo linaloweza kuokoa fedha nyingi kwa ajili ya kuimarisha huduma za jamii kama upatikanaji wa maji safi na salama na pia dawa na vifaa tiba,” chanzo kingine kiliongeza.

Membe alikaririwa hivi karibuni akimpongeza Rais Magufuli kwa kufuta safari holela za nje huku akikiri kuwa wakati wao wakiwa madarakani, viongozi na watendaji wa juu serikalini walikuwa wakipishana angani kwa ndege utadhani nyumbani kunawaka moto.

BILIONI 356/- ZINAWEZA KUFANIKISHA MAMBO HAYA
Uchunguzi uliofanywa na Nipashe umebaini kuwa fedha hizi zilizotafunwa na viongozi mbalimbali kupitia safari za nje (Sh. bilioni 356) zingeweza kufanikisha mambo mengi ya maendeleo kwa taifa.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe hivi karibuni kuhusiana na adha wanazopata wajawazito pindi wanapokwenda kujifungua katika hospitali za serikali ulibaini kuwa hulazimika kuwa na walau Sh. 120,000 ili wajifungue salama.

Fedha hizo ni kwa ajili ya kuwapoza manesi kiasi cha takriban Sh. 60,000 ili kujihakikishia huduma nzuri kama kupata maji ya moto kwa ajili ya kuoga baada ya kujifungua na pia kiasi kingine kwa ajili ya kununulia vifaa kibanio cha kitovu cha mtoto Sh. 500, wembe kukata kitovu cha mtoto Sh. 600, mabomba ya sindano Sh. 600, string injection Sh. 4,500, gloves jozi tano Sh. 17,500, dawa kuzuia damu kutoka Sh. 7,000, dripu moja ya vichocheo vya uchungu Sh. 5,000, mpira wa kulalia, Sh. 10,000 na pamba kubwa Sh.10,000.

Hivyo, kama fedha za safari alizozuia Magufuli kiasi cha Sh. bilioni 356 zitatumika kugharimia kujifungua, maana yake walau kina mama 2,969,367 watanufaika na hivyo kupunguza kero hiyo kwa wananchi katika hospitali za serikali.

MADAWATI 3,098,469
Uchunguzi wa Nipashe hivi karibuni ulibaini kuwa bei ya dawati moja linalochukua wanafunzi watatu wa shule za msingi huwa ni kati ya Sh. 80,000 hadi 150,000, wastani wake ukiwa ni Sh. 115,000. Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha zilizotumika kwa safari za vigogo (Sh. bilioni 356) zingetumika kununua madawati, maana yake yangepatikana madawati 3,098,469 na hivyo kumaliza tatizo hilo katika shule za msingi nchini.

VISIMA VYA MAJI SAFI 35,632
Vyanzo mbalimbali vimeiambia Nipashe kuwa gharama za kuchimba kisima cha maji safi huwa ni kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 100,000 kwa kina cha mita moja, kutegemeana na jiografia ya eneo husika. Kwa sababu hiyo, kama kisima kitakuwa na urefu wa mita 100 na kitachimbwa kwa Sh. 100,000 kwa kila mita moja, maana yake kiasi cha fedha kitakachohitajika ni Sh. milioni 10.

Hivyo, ikiwa fedha za safari za nje (Sh. bilioni 356) zingetumika kuchimba visima vya maji safi vya thamani hiyo, maana yake vingepatikana visima 35,632. Visima hivyo vingegawanywa sawa katika wilaya 133 nchini, maana yake kila wilaya ingepata mgawo wa visima 268.

MIKOPO WANAFUNZI ELIMU YA JUU
Katika uchunguzi wake, Nipashe imebaini kuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayepata mkopo wa asilimia 100 hulipwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jumla ya Sh. 4,219,500 kwa mwaka. Mchanganuo wa mkopo huo kwa mwaka wote wa masomo ni Sh. 2,099,500 kwa ajili ya chakula na malazi, Sh. 200,000 ya vifaa, Sh. 620,000 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ada Sh. milioni 1.3.

Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za safari za nje alizozitaja Rais Magufuli zingetumika kuwapa mikopo wanafunzi wa elimu ya juu kama wa mwaka wa kwanza wa shahada ya uhandisi wa madini wanaolipwa asilimia 100, maana yake wanufaika kwa mwaka wangekuwa wanafunzi 84,447.

MAGARI YA KUBEBEA WAGONJWA
Katika uchunguzi wake hivi karibuni, Nipashe ilibaini kuwa mwaka jana, Agosti 28, kampuni ya Biolands International ilikabidhi msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) aina ya Nissan Patrol kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela lenye thamani ya takriban Sh. milion 76. Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha zilizotajwa na Rais Magufuli kuwa zilitumika kusafirisha vigogo nje ya nchi zingeelekezwa katika kununua magari ya wagonjwa kama walilopata msaada Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, maana yake taifa lingepata magari mapya ya wagonjwa 4,688.

ZAHANATI 4,454.
Akizungumza na Nipashe Septemba 16 mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, January Makamba, alisema kuwa katika jimbo lake, wamekamilisha ujenzi wa zahanati za vijiji kadhaa kwa wastani wa Sh. milioni 80 kwa kila moja. Kwa sababu hiyo, kama fedha za safari alizozitaja Rais Magufuli kuwa zilitumika kusafirisha vigogo nje ya nchi (Sh. bilioni 356) zingetumika kujengea zahanati kama za jimbo la Bumbuli, maana yake taifa lingepata zahanati mpya takriban 4,454.

MAABARA SHULE ZA SEKONDARI 6,122
Mkuu wa Shule ya Sekondari Tandika, Hussein Mpungusi, aliwahi kukaririwa Aprili 20, 2015, akisema kuwa shuleni kwake walikamilisha ujenzi wa maabara mojawapo kwa Sh. milioni 58.2. Kwa sababu hiyo, kama fedha za safari kusafirisha vigogo nje ya nchi wakati wa Rais Kikwete mwaka juzi na mwaka jana zilizotajwa na Magufuli (Sh. bilioni 356) zingetumika kujenga maabara za shule za sekondari kama Sekondari ya Tandika, maana yake zingejengwa maabara 6,122 na kumaliza tatizo hilo nchini.

MIKOPO KWA WAJASIRIAMALI (KILA MMOJA SH. 500,000)
Miongoni mwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali wanawake ni ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao. Hata hivyo, kama ingetokea serikali ya Rais Kikwete ingesitisha matumizi ya fedha za safari za nje kwa viongozi alizozitaja Rais Magufuli (Sh. bilioni 356) na badala yake kuzielekeza katika kuwakopesha mitaji wajasiriamali wanawake kwa kiasi cha Sh. 500,000 kila mmoja, maana yake wanufaika wangekuwa ni kina mama 712,648.

BODABODA AINA YA BOXER
Katika uchunguzi wake hivi karibuni kupitia maduka mbalimbali yanayouza pikipiki jijini Dar es Salaam, Nipashe ilibaini kuwa bei ya juu ya pikipiki aina ya Boxer zinazotumika kwa biashara ya bodaboda ni Sh. milioni 2.5.

Kwa sababu hiyo, ikiwa fedha za posho za safari alizozitaja Magufuli kuwa zilitumika katika miaka ya fedha ya 2013/2014 na 2014/2015 (Sh. bilioni 356) kwa ajili ya safari za vigogo nje ya nchi zingeelekezwa katika kununulia pikipiki hizi kwa ajili ya kuwakopesha vijana wanaotoa huduma ya usafiri wa bodaboda, maana yake zingepatikana pikipiki za aina hiyo takriban 142,530.

VIPIMO CT-SCAN 356
Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa mashine za kipimo maarufu cha CT-Scan, aina ya Phillips huuzwa kwa wastani wa Sh. milioni 600 hadi bilioni moja. Hivyo, kama Sh. bilioni 356.324 alizozitaja Rais Magufuli kuwa zilisafirisha vigogo nje ya nchi zingeelekezwa kununua vipimo hivyo, maana yake zingepatikana CT-Scan 356 za thamani ya Sh. bilioni moja kila moja na kufungwa katika hospitali zote za rufaa nchini na nyingine nyingi zikaelekezwa katika hospitali za wilaya na pia vituo vya afya.

DALADALA TOYOTA COASTER 6,089.
Kwa mujibu wa mtandao wa Trade Car View, bei ya kununua gari aina ya Toyota Coaster iliyotumika lakini iliyo katika hali nzuri ni dola za Marekani 27,896, sawa na takriban Sh. 58,513,255. Kama fedha zilizosafirisha vigogo nje ya nchi katika miaka ya fedha ya mwisho ya Rais Kikwete (Sh. bilioni 356) zingetumika kununulia gari hizi kwa ajili ya kuwapatia wajasirimali wanaotoa huduma ya usafiri wa daladala nchini, maana yake zingepatikana daladala 6,089.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Uchapa kazi wa Magufuli haumhusu Kikwete

Anonymous said...

Ni kweli, lakini makadirio haya yametiwa chumvi, kwa sababu kuna safari zingine ambazo zilikuwa za lazima na gharama zake zilikuwa sehemu ya hayo mabilioni. wachambuzi wangechanganua zaidi ili kujua ni hela kiasi gani ingeokolewa kwa kuondoa safari zote ambazo hazikuwa za lazima/zenye manufaa kwa taifa!