Advertisements

Wednesday, May 20, 2015

Watinga kuchukua maiti wakivalia nguo za magunia

Ndugu na jamaa wa marehemu Victoria Silvester (53), wakiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya KCMC, huku wakiwa wamevaa magunia walipokwenda kuuchukua mwili kwa ajili ya mazishi, mkoani Kilimanjaro jana. Picha na Dionis Nyato.

Moshi. Ilikuwa ni kama kutekeleza maandiko ya Biblia yanayosema “jifungeni nguo za magunia, ombolezeni na kulia kwa uchungu”, wakati ndugu walipokwenda Hospitali ya Rufaa ya KCMC kuchukua mwili wa marehemu.
Walikuwa wamevalia magunia, lakini sababu ya kuvalia nguo hizo haikuwa kama maandiko hayo yanavyosema kuwa “kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha”.
“Tumejiuliza maswali mengi, tumeshindwa kupata majibu. Tumejiuliza tuvae nguo gani hatukupata majibu. Kwa kuvaa hivi tunataka hao wauaji wajue damu hii itawalilia popote walipo,” alisema Beata Kiria, ambaye ni dada wa Victoria Sylvester aliyeuawa na watu wasiojulikana na mwili wake kuzikwa nusu kiwiliwili.
Beata na ndugu zake walifika kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kuuchukua mwili huo wakiwa wamevalia magunia.
Tukio hilo lilitokea jana kati ya saa 4:30 asubuhi na saa 6:00 mchana wakati ndugu hao walipofika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali, huku baadhi yao wakiwa pekupeku na kusababisha watu wengi waliokuwa eneo hilo pamoja na watumishi wa hospitali kuwashangaa.
Wakiwa ndani ya chumba cha kuhifadhia maiti, ndugu hao walilia wakipaza sauti wakitaka wauaji wa mwanamke huyo wakamatwe kabla ya kuchukua mwili na kuondoka nao.
Victoria (53), mkazi wa Kijiji cha Masherini, Umbwe eneo la Kibosho aliuawa kwa kukatwa mapanga usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita na baadaye wauaji kuuzika mwili wake nusu na kuacha kiwiliwili nje ya nyumba waliyokuwa wakiishi, jambo lililoibua utata mkubwa ndani ya familia hiyo.
Akizungumza na gazeti hili, Kiria alisema walichagua mavazi hayo baada ya kukosa vazi lingine.
“Tulitafakari tuvae nguo gani ili kumuenzi marehemu lakini hatukupata jibu, ndiyo tukaamua tuvae magunia kuonyesha kuwa waliomuua ndugu yetu thamani yao inafanana na magunia haya,” alisema Kiria.
Imezoeleka misiba mingi ndugu huvaa suti nyeusi kwa wanaume huku wanawake wakivalia mavazi meusi au meupe ambayo baadaye hujifunika na vitambaa vyeusi au vyeupe kwa akina mama.
Kiria, ambaye alizungumza kwa niaba ya familia, alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawatafuta na kuwakamata watu waliohusika na mauaji hayo.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema wanamshikilia mume wa marehemu, Silvester Mmasi na mtumishi wao ambaye hakumtaja kwa ajili ya mahojiano kuhusu mauaji hayo na polisi inaendelea kuwatafuta washukiwa wengine.
MWANANCHI

No comments: