Advertisements

Wednesday, September 10, 2014

Kikwete awatimua makada wa CCM waliokusanyika kumpokea

  Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipata maelezo wakati alipokagua wodi maalumu iliyotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa ebola iliyoko katika eneo la hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana aliwafukuza makada wa CCM waliokuwa wakimsubiri kwenye kituo cha dharura cha ebola alipokitembelea kwa kushtukiza katika Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Makada hao ambao baadhi yao walivalia sare za CCM, kinyume na matarajio yao, kiongozi huyo alipofika hospitalini hapo alionyesha kuwashangaa kabla ya kuwataka waondoke kwa kuwa hakuhitaji kuzungumza nao, bali wasimamizi wa kituo hicho.
“Hawa watu wote wanafanya nini hapa! Sijaja kuhutubia hapa mimi. Ndugu zangu hawa waliowaita wamewasumbua bure, nawashukuruni sana kwa kuja, endeleeni na shughuli zenu,” alisema Rais Kikwete ambaye aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki.
Hatua hiyo ilionekana kuwanyong’onyeza makada hao ambao hawakuwa na jinsi isipokuwa kuondoka taratibu kwenye eneo hilo na kumwacha Rais Kikwete na viongozi wa kituo hicho.
Ukaguzi wa kituo
Katika ukaguzi wa kituo hicho, Rais Kikwete alieleza kutoridhishwa na maandalizi na akaagiza ukarabati mkubwa ufanywe haraka ili kiwe na hadhi inayostahili.
Alionyesha kushangazwa na miundombinu duni ikiwamo vyoo vibovu na ukosefu wa maji katika kituo hicho na kuagiza kufanyika marekebisho ya haraka.
“Hivi hii ni kweli? Hakuna maji, vyoo vibovu, kituo chenyewe kikuukuu! Kwa taarifa za awali, kituo hiki kilikuwa ni kwa ajili ya ugonjwa wa kipindupindu, hakiendani kabisa na hitaji la sasa la kuwahudumia wagonjwa wa ebola iwapo watabainika kuingia nchini,” alisema Rais Kikwete.
Alisema katika hali ya kawaida, kituo hicho kinatakiwa kuwa cha kisasa na chenye mazingira yanayowezesha kutoa huduma kwa wagonjwa hao kwa usalama.
Alisema ameamua kufanya ziara hiyo Temeke na ukaguzi wa namna Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuona ukweli wa taarifa alizopewa na kuzizungumza katika mkutano na wazee wa Mkoa wa Dodoma wiki iliyopita.
“Hii ndiyo fursa ya hii dharura ambayo mnatakiwa kuitumia vyema na kupata kituo cha kisasa na kwa wakati huu. Kama kuna matatizo ya fedha tuelezane tutajua namna ya kufanya,” alisema Rais Kikwete.
Alisema ni vyema kuhakikisha kunakuwa na kituo maalumu cha kuwapokea na kuwahifadhi waathirika wa magonjwa ya mlipuko ambacho ni cha kipekee na cha aina yake nchini.
Mratibu wa Huduma za Dharura wa Mkoa wa Dar es Salaam, Christopher Mnzava alisema kituo hicho kimeandaliwa na manispaa zote tatu za Jiji la Dar es Salaam; Temeke, Ilala na Kinondoni.
Alisema tayari kamati maalumu iliyoundwa Agosti 5, mwaka huu chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa imeangalia maeneo muhimu ya kufanyia kazi, ambayo ni suala la tiba, namna ya kuwahifadhi wagonjwa, usafiri wa wagonjwa, utoaji wa mafunzo kwa watumishi na jamii ya Mkoa wa Dar es Salaam
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema wizara yake inasimamia pia uanzishwaji wa vituo vya aina hiyo kwa ajili ya dharura katika kila mkoa ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema pia inafanya mpango wa kuimarisha maabara ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Tiba (NIMR) ili iwe na uwezo mkubwa wa kupima magonjwa mengi ikiwamo ebola.
Mwananchi

No comments: