Advertisements

Friday, September 21, 2012

BALOZI WA KUDUMU WA TANZANIA UMOJA WA MATAIFA AWASILISHA HATI ZAKE KWA KATIBU MKUU WA UMIOJA WA MATAIFA(UN) BAN KI MOON


  Katibu Mkuu akiwa na Balozi Manongi mara baada ya kupokea hati hizo za utambulisho.

   Katibu Mkuu  wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akisalimiana  na Balozi Tuvako N. Manongi, Balozi wa Kudumu wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa  kabla ya kukabidhi hati zake za Utambulisho.
Balozi Tuvako Manongi, akiwa katika picha ya pamoja na  maafisa na wafanyakazi wa Ubalozi mara baada ya kuwasilisha hati za Utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.Picha na Mpiga picha Maalum

NA MWANDISHI MAALUM, UN
Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika  Umoja wa Mataifa,  Tuvako  N. Manongi jana Jumatano amewasilisha hati zake za utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon.

Balozi Manongi alikuwa kati ya  Mabalozi Sita waliowasilisha hati zao siku hiyo ya jumatano ikiwa ni  siku chache kabla ya kuanza  kwa Mkutano wa  67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaowahusisha Wakuu wa Nchi  na Serikali kutoka nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa.
Hafla ya kukabidhi hati hizo imefanyika Ofisini kwa Katibu Mkuu na kushuhudiwa na  baadhi ya Maafisa Waandamizi kutoka Ubalozini .
Baada ya kukabidhi hati hizo, Katibu Mkuu Ban Ki Moon alifanya mazungumzo na Balozi Tuvako Manongi.
  Katika mazungumzo hayo,  Katibu Mkuu amesema anaendelea kuitegemea   Tanzania  kama  nchi kiongozi na mshawishi katika kusukuma mbele ajenda zake, zikiwamo zile zinazolenga kufanya  mapitio  ya baadhi ya majukumu ya Umoja wa  Mataifa.
  Akasem.“Ninayo mahusiano   ya karibu na  ushirikiano mzuri sana na  Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Nje Bernard  Membe  na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wangu Asha-Rose Migiro. Mimi na wewe tunafahamiana vizuri tumefanya kazi kwa karibu.  Ninakutumainia wewe  na nchi yako kwamba mtaendelea kuwa msaada kwangu  na kushirikiana nami kwa karibu” akasititiza Ban Ki Moon.
Aidha Katibu Mkuu huyo wa UM , ambaye alionyesha wazi  kufurahishwa na  Uteuzi wa Balozi Manongi kuwa Balozi katika  Ubalozi wa Kudumu  wa Tanzania katika UM,  na hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa mmoja wa  maafisa wake waandamizi  kabla ya uteuzi huo. Na  amemhakikishia  Balozi   ushirikiano wa karibu  na kwamba milango iko wazi wakati wowote akimhitaji.
Kwa  upande wake, Balozi Manongi pamoja, na kufikisha kwa Katibu Mkuu Salamu rasmi alizotumwa na Mhe. Rais Jakaya Kikwete  amesema, atatumia uzoefu wake kusukuma mbele ajenda si tu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa bali  pia hasa zile ambazo zina maslahi kwa  Jamhuri  ya  Muungano wa Tanzania na  Afrika kwa Ujumla.
Sehemu ya  salamu rasmi za  Mhe.  Rais Jakaya Kikwete kwa Ban  Ki Moon, zilikuwa ni pamoja na kumshukuru Mkuu huyo wa UM kwa uamuzi wake wa kuitisha mkutano  maalum  utakaojadili   mgogoro na  kuzotora kwa   usalama na amani katika  eneo la Mashariki ya  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC).
  Mkutano  huo  utawashirikisha viongozi mbali mbali wakiwamo wakuu wa Nchi na Serikali na wadau wengine  kujadiliana  ambapo watajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu  namna bora ya kuchagia upatikanaji wa amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya  Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano huo utafanyika   Septemba 27 hapa  Umoja wa Mataifa na unatarajiwa kutoka na tamko rasmi.
Ikumbukwe  pia kwamba, Rais Jakaya Kikwete  ni  Mwenyekiti wa  Asasi ya  Siasa,   Ulinzi  na  Usalama ya  Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za   Kusini mwa Afrika ( SADC) na amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu  na amani ya kudumu katika eneo hilo na  Mashiriki ya DRC.
Balozi  Tuvako  Manongi anakuwa  Balozi wa  kumi na Nne  (14) tangu kuanzishwa rasmi kwa Ubalozi wa Kudumu wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa.
Mabalozi wengine ambao wamewahi  kushika wadhifa huo huko nyuma, ni  Balozi Vedast K. Kyruzi, Balozi A.Z. Nsilo Swai, Balozi Chifu Erasto A.M. Mang’enya, Balozi John W.S. Malecela, Balozi Akil B.C. Daniel, Balozi Salim Ahmed Salim, Balozi Paul M. Rupia, Balozi Mohamed Ali Foum, Balozi  Dr.Wilbert K. Chagula, Balozi Anthony B. Nyaki, Balozi Daudi N. Mwakawago, Balozi Dr.Augustine P. Mahiga,  na Balozi Ombeni Y. Sefue.
  Balozi  Manongi   atafanya kazi kwa karibu na  kwa ushirikiano  mkubwa na Naibu Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi anayetarajiwa kuwasili kituoni wakati wowote.

No comments: